Loading...

PICHA ZOTE ZA MAZISHI YA BRIGEDIA JENERALI MBITA, JK AMLILIA


 

Mwili wa Brigedia Jenerali Hashim Mbita ukiswaliwa Msikitini.

Mwili wa Marehemu Mbita ukiingizwa kwenye gari maalum la Jeshi kwa ajili ya kupelekwa makaburi ya Kisutu Dar kwa maziko.

Safari ya kuelekea makaburini kwa ajili ya maziko ya Mbita.

Rais Mstaafu wa awamu ya tatu wa Tanzania, Benjamin William Mkapa akiwa katika jukwaa lililokuwa limeandaliwa katika Makaburi ya Kisutu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (wa nne kushoto) akiwa katika jukwaa lililoandaliwa katika makaburi ya Kisutu.

Brasbendi ya JWTZ ikiongoza maandamano ya waombolezaji katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.

Majenerari wastaafu (kushoto) wakiongozwa na Mnadhimu Mkuu wa JWTZ Luteni Jenerali Samweli Ndomba aliyevaa kombati wa tatu kulia.

Maafisa wa JWTZ wa vyeo vya Meja wakipeleka mwili wa Marehemu Brigedia Mbita Kaburini.

Wanajeshi wa JWTZ wakiwa kwenye paredi maalum la mazishi ya Brigedi Mbita katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam jana.

Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Ulinzi na Usalama Dkt. Jakaya Kikwete akitoka kuweka udongo kwenye kaburi la Marehemu Brigedia Mbita kama inavyoonekana pichani.

HATIMAYE mamia ya wananchi wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete jana walijitokeza kumzika aliyekuwa Katibu wa Kamati ya Ukombozi kwa nchi za Kusini mwa Afrika, Brigedia Jenereli Mstaafu Hashim Mbita.

Kabla ya kuzikwa kwenye makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam, mwili wa marehemu Mbita ulifikishwa katika msikiti wa Kwa Mtoro Kariakoo kwa swala maalum ya mazishi.

Marehemu Brigedia Jenerali Hashim Mbita alizaliwa Novemba 2, 1933 katika kijiji cha Songoro, mkoani Tabora. Katika utumishi wake alishika nyadhifa mbalimbali, ikiwemo Ofisa Habari Mkuu wa Serikali mwaka 1962 hadi 1965 na mwandishi wa habari wa rais 1965 hadi 1967.

Marehemu Mbita pia enzi za uhai wake aliwahi kuwa Mwalimu wa siasa katika Chuo cha Kijeshi cha Monduli mwaka 1969 hadi 1970, Katibu wa Kamati ya Ukombozi Kusini mwa Afrika, 1972 hadi 1989 na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe kuanzia 2003 hadi 2006. Brigedia Jenerali Hashim Mbita alifariki dunia Aprili 26 mwaka huu katika hospitali ya Jeshi ya Lugalo na alizikwa jana katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam

BREAKING NEWZ,,,, VURUGU ZAZUKA NCHINI BURUNDI BAADA YA RAIS NKURUNZIZA KUTEULIWA KUGOMBEA TENA URAIS





Waandamanaji wakiwa Mjini Bujumbura.

Kumezuka ghasia katika Mji wa Bujumbura nchini Burundi kati ya maofisa wa polisi na waandamanaji wanaoishutumu serikali kwa kufanya mapinduzi ya kikatiba.

Waandamanaji walirusha mawe na kuchoma matairi huku maofisa wa polisi wakilazimika kurusha mabomu ya machozi hewani.

Ghasia hizo zinafuatia tangazo la jana kwamba Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza ameteuliwa na chama chake kuwania muhula wa tatu wa urais.

Upinzani umeitaja hatua hiyo kama ukiukaji wa katiba na kuonya kuwa huenda ikaathiri makubuliano ya amani ambayo yalimaliza miaka kadhaa ya mapigano ya kikabila.

Serikali imesema kuwa maandamano hayo si halali.

Maelfu ya raia wa Burundi wamelitoroka taifa hilo katika majuma ya hivi karibuni wakihofia kuongezeka kwa ghasia hizo huku taifa hilo likijiandaa kwa uchaguzi utakaofanyika Mwezi Juni mwaka huu.

ZITTO SPIDI 120




Na Elvan Stambuli
MWENDO wa Kiongozi Mkuu wa Alliance for Change and Transparency (ACT) Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe (pichani) umetafsiriwa kuwa ni wa spidi 160 kutokana na kujawa wasikilizaji katika mikutano yake anayofanya kwenye mikoa mbalimbali nchini.

Kiongozi Mkuu wa Alliance for Change and Transparency (ACT) Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe.

Zitto ameshafanya mikutano katika Mikoa ya Ruvuma, Njombe, Morogoro, Shinyanga na Mwanza na mikutano yake imekuwa ikihudhuriwa na wananchi wengi, hivyo kutumia mwanya huo kugawa kadi za chama chake.
Alipohojiwa na gazeti hili kuhusu hali hiyo ya kujaza watu, Zitto alisema mwendo wa chama chake ni kama moto wa pumba ambao ukiwa unauangalia kwa juu, utadhani umezimika lakini ukiingiza mguu, unaungua.
“Sisi tunafanya kazi usiku na mchana ili kupata wanachama ili uchaguzi mkuu ukifika tupate wabunge wa kutosha,” alisema Zitto aliyewataka wananchi kujiandikisha muda ukifika pale Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) itakapowafikia kuwaandikisha.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa alipoulizwa kama spidi 160 anayokwenda nayo Zitto haiwezi kuwa tishio kwa chama chake, alisema Chama cha ACT Wazalendo hakiwezi kukitisha chama chake hata kidogo.
Dk. Slaa aliongeza: “Chadema tumeijenga kuanzia ngazi za chini kwa miaka mingi, hatumuogopi yeyote. Dk. Slaa, Mbowe na timu nzima tumezunguka Tanzania nzima kijiji kwa kijiji, hivyo hakuna mtu yeyote atakayekuwa tishio kwetu.”
Akizungumzia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), alisema imekuwa ikilalamikiwa kuhusiana na kuchelewa kuletwa kwa mashine za mfumo wa Biometric Voters Registration ( BVR), lakini dosari ya msingi katika suala la BVR ni serikali kushindwa kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivyo.
Dk. Slaa alisema Agosti 30 na Septemba 8, mwaka jana, viongozi wa vyama vya siasa nchini walikutana na Rais Jakaya Kikwete na wakajadiliana masuala kadhaa likiwamo la uandikishaji wa Daftari la Wapiga kura kwa kutumia mfumo mpya wa BVR na kukubaliana kuwa mambo ambayo siyo ya kikatiba na yasiyo ya lazima yasifanyike kwanza katika kipindi hiki ili kupunguza gharama.
Dk. Slaa ambaye amerejea hivi karibuni kutoka Marekani, alisema miongoni mwa mambo waliyoyaomba yasifanyike kwanza ni kura ya maoni kwa ajili ya Katiba Inayopendekezwa kwa kuwa siyo jambo la kikatiba, lakini katika hali ya kushangaza serikali ikatangaza tarehe ya kufanyika kura ya maoni licha ya kuwapo makubaliano hayo.
“Rais Kikwete alikubali na kupendekeza kuahirishwa kura ya maoni hadi baada ya uchaguzi mkuu ili kuokoa fedha ili zitumike kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, lakini hilo halikuzingatiwa,” alisema.
Aliongeza kuwa hadi sasa serikali imetumia fedha nyingi sana kufanya kampeni kwa ajili ya kura ya maoni na cha kushangaza ni kuwa serikali ndiyo inayofanya kampeni badala ya wananchi .
Dk. Slaa alisema wamebaini kuwa kuandikisha wapiga kura kwa kutumia BVR ni mbinu inayofanywa na serikali kwa sababu kuna maeneo ambayo wananchi hawataandikishwa na ndiyo maana wameanza maeneo ambayo ni ngome za Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Tunataka kuwaambia kuwa tumeshtukia na tunatoa rai kwa Rais Kikwete, nchi hii ni muhimu kuliko yeye, nchi ni muhimu kuliko CCM na kuliko Chadema, hata siku moja upinzani hauwezi kuleta vurugu, vurugu zitaletwa na serikali yenyewe inayotaka kulazimisha mambo yake,” alisema.

CHADEMA NUSURA WAMUUE CHENGE




Na Mwandishi Wetu
Kimenuka! Wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mjini Bariadi, Simiyu, juzi almanusra wayakatishe maisha ya mbunge wa jimbo hilo, Mheshimiwa Andrew Chenge (pichani) baada ya kuvamia msafara wake, hali iliyolazimu risasi zitumike kumuokoa.


Mh. Andrew Chenge

Kwa mujibu wa habari zilizotua kwenye dawati la Uwazi Mizengwe, tukio hilo la aina yake, lilitokea mishale ya saa moja kasoro za jioni, Jumatano ya Aprili 22, 2015 kwenye eneo maarufu la Mwisho wa Lami zilipo ofisi za Chadema wakati Chenge na wafuasi wake wakirejea kutoka kwenye mkutano wa hadhara.
“Yaani ni Mungu tu, hivi sasa tungekuwa tunazungumza mengine kuhusu Mheshimiwa Chenge, wafuasi wa Chadema wangemuua,” alisema shuhuda wa tukio hilo aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini na kuongeza:
“Unajua siku hiyo kulikuwa na mikutano miwili ya hadhara, mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika eneo la Isanga na kuhutubiwa na Mheshimiwa Chenge na mwingine wa Chadema uliohutubiwa na John Mnyika na Heche.
“Mikutano yote iliisha salama na wafuasi wa Chadema wapatao 2,000, wakawasindikiza viongozi wao kwenda kwenye ofisi za Chadema zilizopo Mwisho wa Lami, kandokando ya Barabara ya Maswa- Lamadi,” alisema shuhuda huyo na kuendelea kuongeza kuwa walipofika kwenye ofisi hizo, waliendelea kuimba na kushangilia na kutawanyika mpaka barabarani.
“Ghafla msafara wa Chenge ukafika eneo hilo huku muziki ukisikika kwa sauti kubwa ndani ya gari moja, wafuasi wote wa Chadema wakiwa wameshika mawe wakauzingira na kuanza kuzomea. Mara Chenge na wafuasi wake wakateremka chini, hapo ndipo kiliponuka.
“Mtu mmoja aliwaamrisha wafuasi wa Chadema kuanza kuwapiga mawe watu wote, akiwemo Chenge, kukatokea bonge la mtiti, Chenge na wenzake wakawekwa ‘mtu kati’ na kutaka kushushiwa kichapo.

MILIO YA RISASI
“Ghafla ikasikika milio ya risasi tatu, watu wote wakatawanyika huku wengine wakikanyagana na kuwapa mwanya Chenge na wenzake kukimbilia kwenye magari yao na kutokomea kusikojulikana, yaani ilikuwa kama filamu ya mapigano vile, aisee,” alisema shuhuda huyo.


Baada ya kupata habari hizo, Uwazi Mizengwe liliwatafuta Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika na Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) John Heche kutaka kujua kilichotokea.
Kwa mujibu wa Mnyika, wao walikuwa kwenye ofisi za Chadema lakini ghafla walivamiwa na msafara wa Chenge ukiwa kwenye magari zaidi ya sita huku wakiwa wanapiga muziki kwa sauti kubwa na kuanza kufanya vurugu kabla ya mtu mmoja kwenye msafara huo kuchomoa bastola na kufyatua risasi.

“Ni kweli, ilikuwa ni baada ya mkutano mkubwa viongozi wa Chadema, walisindikizwa na wananchi mpaka kwenye ofisi zetu, Chenge na wenzake wakaamua kuja jirani na ofisi hizo na kufyatua risasi kuwatawanya wananchi,” alisema Mnyika na kumtaka mwandishi awasiliane na Heche ambaye ndiye aliyeenda kuandikisha maelezo kituo cha polisi.
Uwazi lilimtafuta Heche kwa njia ya simu na alipopatikana, alitoa maelezo ambayo hayatofautiani na Mnyika.


“Chenge na wafuasi wake walituvamia ofisini kwetu na kuanza kuleta fujo, ghafla tukashangaa wanatufyatulia risasi, ikabidi wafuasi wa chama chetu wakimbie kuokoa maisha yao,” alisema Heche na kuendelea kueleza kuwa baada ya tukio hilo, walikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Bariadi na kupewa RB yenye namba BAR/RB/1195/2015.
“Cha ajabu tulipofika kituoni, tulimkuta Chenge na wafuasi wake nao wamekuja kutoa taarifa,” alisema Heche.

CHENGE SIMU YAKE VP?
Uwazi Mizengwe halikuishia hapo, lilimtafuta Chenge ambaye muda wote simu yake haikuwa ikipatikana hewani. Likaamua kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, ACP Gemini Mushi ambaye alikiri kutokea kwa tukio hilo.

ASEMAVYO RPC
“Taarifa zilizopo ni kwamba Mheshimiwa Chenge na wenzake walikuwa wakitoka kwenye mkutano halali walioufanya eneo la Isanga, sasa wakati wanarudi wakapita kwenye ofisi za Chadema zilizopo Mwisho wa Lami ambapo wafuasi wa Chadema waliwavamia na kusababisha vurugu kubwa.
“Katika kujihami, mtu mmoja aliyekuwa kwenye msafara wa Chenge aitwaye Ahmed Ismail alifyatua risasi tatu hewani, ndipo wakapata upenyo wa kukimbia baada ya wafuasi wa Chadema kutawanyika.
“Mkanganyiko uliopo ni kwamba CCM wanasema Chadema ndiyo waliowavamia, Chadema nao wanasema CCM ndiyo waliowavamia, hivyo hali ni tete. Tunaendelea kulichunguza tukio hilo,” alisema Kamanda Gemini na kuongeza:
“Wanasiasa wajifunze kupambana kwa hoja wawapo kwenye majukwaa ya siasa lakini siyo kupigana kwa mawe au bastola.”
Kamanda huyo aliongeza kuwa baada ya kufanya uchunguzi, walibaini kwamba bastola iliyotumika, ilikuwa ikimilikiwa kihalali na Ahmed na kwamba hakukuwa na mtu yeyote aliyejeruhiwa.

Haya Ndio Maisha aliyopitia Mh January Makamba Toka Anazaliwa Mpaka Hapo Alipofikia!





Nilizaliwa tarehe 28 Januari 1974 mjini Singida, kwa Bi. Josephine Joseph na Bwana Yusuf Makamba. Mwaka 1978, nilipelekwa kuishi kijijini kwa bibi mzaa mama Kyaka, Kagera wakati mama ameenda kuendelea na masomo ya uuguzi. Kijijini kwetu ilikuwa umbali mfupi kutoka Mutukula, mpakani mwa Tanzania na Uganda. Idi Amini alipovamia Tanzania mwaka huo, kitongoji chetu kinachoitwa Kituntu, sio Kituntu ya Karagwe unayoijua wewe Padre, karibu na Kyaka nacho kilipigwa mabomu. Mimi na bibi yangu tulikimbia makazi yetu na kuhamia kwenye kambi ya wakimbizi eneo linaloitwa Mwisa. Baba yangu wakati huo alikuwa mstari wa mbele kwenye vita dhidi ya Idi Amin. Tulikaa kambini kwa muda baadaye tukafanyiwa utaratibu wa kuondoka kwenda Biharamulo na mama akaja kutuchukua. Sina kumbukumbu kubwa sana ya kipindi hiki kwa kuwa nilikuwa bado mdogo ila nakumbuka mvua nyingi, milio ya ndege na mabomu.

Nimesoma shule nne za msingi katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu kutokana na wazazi kuhamishwa mara kwa mara katika utumishi wa umma. Lakini pia kuanzia darasa la tatu hadi la tano nilirudishwa tena kijijini, Kituntu Kyaka, kukaa na bibi. Maisha ya kijijini siwezi kuyasahau. Enzi hizo, miaka ya mwanzoni mwa 1980, maisha ya kijijini yalikuwa magumu sana, bidhaa muhimu kama sukari, sabuni, dawa za mswaki, chumvi, na nyinginezo, zilikuwa adimu. Kutoka kitongojini Kituntu hadi shuleni ilikuwa mwendo mrefu na baada ya shule nilikuwa na kazi ya kwenda kuchunga mbuzi wa bibi, na baada ya kuchunga mbuzi kila jioni saa moja ilikuwa ni kazi ya kuchota maji mtoni, na baada ya hapo ilikuwa ni kumsaidia bibi kuuza pombe ya lubisi usiku na Jumamosi ilikuwa ni kwenda shamba kupalilia migomba na mikahawa. Maisha yale yalinifundisha mambo mengi. Baada ya miaka mitatu, nilirudi kukaa na wazazi na kumalizia darasa la saba Shule ya Msingi Masiwani, Tanga Mjini.

Nilianza Sekondari katika shule ya Sekondari Handeni, Tanga. Nakumbuka wakati naanza pale shule ile ilikuwa bado inajengwa, sisi tulikuwa Form 1 wa pili na ilikuwa haina tofauti kabisa na shule ambazo sasa zinaitwa shule za Kata. Kwa kuwa hii ilikuwa shule ya kutwa, mzazi wangu alipohamishwa kikazi kutoka Handeni, nikahamia Shule ya Sekondari Galanos Tanga, ambayo ilikuwa shule ya Serikali ya boarding.

Nilikuwa mwanafunzi mzuri pale Galanos, na, nikiwa kidato cha tatu, nikachaguliwa kuwa Makamu wa Kiranja Mkuu. Nilikuwa nafanya vizuri darasani, nikachagua mchepuo wa sayansi nikiwa na combination ya Chemistry (Kemia), Biology (Baiolojia) na Agriculture (Kilimo) (CBA). Nilipata daraja la kwanza kwenye mtihani wa kanda wa mock wa kidato cha nne, nikiwa na uhakika wa kuendelea na A-Level katika Shule ya Sekondari Kibaha, shule pekee iliyokuwa inafundisha mchepuo wa CBA hapa nchini. Hata hivyo, nilifanyiwa hujuma kubwa kutokana na siasa zinazomhusu Mzee wangu na kufutiwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne.

Sikufa moyo, nilirudia mtihani kama mtahiniwa binafsi na kufaulu na kuweza kusoma A-Level katika Shule ya Sekondari Forest Hill Morogoro na nikapata Daraja la Pili kwenye mtihani wa Kidato cha Sita. Kabla ya kwenda Chuo Kikuu, niliamua kwenda kufanya kazi kwenye makambi ya wakimbizi kutoka Burundi yaliyokuwa wilaya ya Kasulu, Mkoani Kigoma. Niliipenda sana kazi ile ya kuhudumia wakimbizi na kuifanya kwa bidii kubwa. Nilipewa madaraka zaidi hadi kufikia nafasi ya Meneja wa Kambi Msaidizi wa Kambi ya Mtabila 2 iliyokuwa na wakimbizi zaidi la laki moja. Nilibahatika kuwa na wajibu na dhamana kubwa ya kuongoza kambi kubwa na wafanyakazi wengi nikiwa na umri mdogo tu wa miaka 21. Nilikuwa na wafanyakazi wengi, tena wengine watu wazima, waliokuwa wanaripoti kwangu. Nilikuwa na wajibu wa kuhakikisha kwamba wakimbizi laki moja wanapata viwanja vya kuishi, wanapata vifaa muhimu kama mahema, na wanapata chakula. Kazi ile ilibadilisha kabisa mtazamo wangu juu ya maisha. Baada ya kushuhudia adha wanayopata wanadamu wenzetu kutokana na vita hadi kukimbia makazi yao na nchi yao na kuja kukaa maporini kwenye nchi yetu, na baada ya kutafakari kuhusu udhalilishwaji na mateso yanayotokana na ukimbizi, niliamua kuachana na azma ya kusoma sayansi na uchumi na nikaamua kwamba maisha yangu nitayatoa katika kuchukua masomo kuhusu amani, na namna ya kutafuta amani ili nitoe mchango kwenye kuepusha vita na kupatikana kwa amani duniani. Hivyo, nilianza kutafuta vyuo duniani vinavyofundisha masuala ya amani. Nilipata chuo kimoja cha Wakatoliki Marekani, kinachoitwa St. John University. Lakini kilikuwa Chuo aghali kidogo, kwa hiyo nikaanza kusoma masomo ya awali kwenye Chuo kingine kidogo katika jiji la Boston kinachoitwa Quincy College na baadae nikajiunga na St. John University na kupata shahada ya kwanza ya sayansi ya masomo ya amani (Bachelor of Science in Peace Studies). Gharama za masomo zilikuwa kubwa na nilihangaika kufanya kazi mbalimbali, ikiwemo kazi za ulinzi na kuhudumia watu wenye magonjwa ya akili ili kulipia ada ya shule.

Baada ya kumaliza shahada ya kwanza, nilishinda tuzo ya kujiunga na taasisi ya Rais Mstaafu wa Marekani, Jimmy Carter, inayoitwa Carter Presidential Center iliyopo Atlanta hukohuko Marekani. Ilikuwa changamoto kubwa na fursa nzuri kwa sababu vijana wote waliojiunga pale walikuwa ni vijana mahiri sana na wenye uwezo mkubwa. Taasisi ile ilinipeleka nchini Sierra Leone kusimamia uchaguzi mkuu na kutekeleza mradi wa kufufua taasisi za haki zilizoporomoka baada ya vita. Nako pia nilijifunza mengi kuhusu ujenzi wa taifa.

Baada ya hapo nikaamua kuchukua shahada ya pili (Masters degree) kwenye Chuo Kikuu cha George Mason kilichoko Jimbo la Virginia, Marekani. Nilipata wakati mgumu kulipa ada, kiasi cha kukaribia kufukuzwa shule. Niliomba msaada kwa watu mbalimbali akiwemo Rais wa wakati ule Mhe. Benjamin William Mkapa. Bahati nzuri, alikubali kusaidia kwa sharti kwamba nije kutumia utaalamu wangu Serikalini nitakapomaliza masomo. Na ndivyo nilivyofanya. Baada ya masomo hayo, nikajiunga na Wizara ya Mambo ya Nje.

Mwaka 2005 nilifunga ndoa na mchumba wangu wa miaka minne, Ramona Urasa, na nimekuwa na familia yenye furaha sasa mwaka wa kumi. Pale Wizarani, nilipata fursa ya kufanya kazi na Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete. Nahisi alipenda kazi zangu na mara alipoamua kuwania nafasi ya Urais akanitaka nichukue likizo isiyo na malipo Serikalini ili niwe msaidizi wake kwenye kampeni zile. Siwezi kusahau maishani mwangu ile fursa kubwa kwani niliweza kuijua kwa kina nchi yangu na watu wake. Na kwa kuwa kampeni zinahusu ahadi za utatuzi wa kero za watu, nilipata fursa ya kujua kero za Watanzania kwenye kila wilaya ya nchi yetu.

Baada ya Rais Kikwete kushinda aliniteua kuwa Msaidizi wake Ikulu, nikiwa na jukumu la kumsaidia kuandika hotuba zake, pamoja na mambo mengine mengi ya uendeshaji wa shughuli zake za kila siku. Kazi ile ilikuwa ngumu kwa sababu inakulazimisha kujifunza na kujua karibu kila kitu ndani ya Serikali na duniani kwa ujumla, na kufanya utafiti karibu kila siku kwa sababu Rais anazungumza kila siku kuhusu mambo mbalimbali na kwa makundi mbalimbali. Pia kazi ile inakupa fursa ya kuhudhuria vikao vya Baraza la Mawaziri kama msikilizaji ambapo pia unajifunza mambo mengi ya uendeshaji wa Serikali, ikiwemo maamuzi muhimu ya kisera na kiutendaji yanavyofanywa. Ni nafasi ya heshima sana na sitamsahau Rais Kikwete kwa kunipa fursa ile.

Baba yangu alikuwa mwanasiasa karibu maisha yake yote lakini sikupata kuwaza kuingia kwenye siasa katika maisha yangu hadi nilipofanya kazi na Rais Kikwete. Baada ya kufanya kazi ile Ikulu kwa miaka mitano, nami nikahamasika na kuamua kushiriki katika uongozi wa umma. Niliamua kwenda kwetu Bumbuli kugombea nafasi ya Ubunge mwaka 2010, nikafanikiwa. Baada ya kuingia Bungeni nikapata nafasi ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini. Kazi ile tuliifanya vizuri sana na wenzangu kwenye Kamati hasa katika kipindi kile kigumu cha mgao wa umeme na matatizo ya mafuta nchini.

Baada ya kitambo kidogo, nikateuliwa kwenye Sekretarieti ya Chama nikiwa kama Katibu wa NEC wa Siasa na Mambo ya Nje, na nikawa Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM. Nilishika nafasi hizi katika kipindi kigumu sana kisiasa kwa Chama chetu na nilijifunza mambo mengi na kutoa mchango wangu kwenye kukijenga na kukiimarisha. Baada ya kitambo kingine, nikateuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.

Kuhusu kubebwa na jina la mzazi, kama nilivyosema hapo awali, pamoja na kwamba mzazi wangu alikuwa kwenye siasa kwa muda mrefu, binafsi, ingawa nilipenda na nilishiriki kuwa kiongozi tangu shuleni, sikuwa na mawazo ya kuingia katika siasa. Nilipokuwa Sekondari nilipenda kuwa mwanasayansi wa kilimo.

Baada ya kuzunguka nchi nzima kwenye kampeni ya 2005 na baada ya kufanya kazi ya kumsaidia Rais Ikulu ndipo nilipobaini kwamba siasa, ukiiendesha vizuri na kwa manufaa ya watu, inayo nafasi ya kubadilisha maisha ya watu. Nilipofanya uamuzi wa kugombea Ubunge, sikutaka ushauri wa baba yangu kwa sababu nilikuwa na uhakika kwamba angenikatalia. Niliamua mwenyewe na nikaanza harakati na ndipo nikamwambia. Kwa hiyo, unaweza kuwa na mzazi mwanasiasa na bado ukaweza kuwa na uhuru wa kujiamulia mwenyewe unataka kufanya nini.

Ni kweli kwamba jina maarufu la mzazi aliye kwenye siasa linasaidia kwa maana tayari kuna watu ambao wanamheshimu na ambao wapo tayari kukusaidia. Lakini pia jina hilohilo linaweza kukuharibia kwa sababu pia unaweza kurithi maadui zake, ambao wanakuona wewe ni sehemu ya yeye hata kama una mawazo na mtizamo huru. Kwa hiyo, siasa yangu nimejitahidi kuifanya kama mimi binafsi. Mimi na baba yangu tuna staili tofauti za siasa na mimi nina namna yangu ya kufanya mambo ambayo inatofautiana na yake. Lakini pia kuna mambo mengi mazuri ambayo nimejifunza kutoka kwake ikiwemo haja ya kuwa na msimamo usioyumba katika unayoyaamini na haja ya kutokumuogopa mtu yoyote.
Older Posts
© Copyright Bongo Mirror | Designed By BONGOJAMII.COM
Back To Top