Na Mwandishi Wetu
Kimenuka! Wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mjini Bariadi, Simiyu, juzi almanusra wayakatishe maisha ya mbunge wa jimbo hilo, Mheshimiwa Andrew Chenge (pichani) baada ya kuvamia msafara wake, hali iliyolazimu risasi zitumike kumuokoa.
Mh. Andrew Chenge
Kwa mujibu wa habari zilizotua kwenye dawati la Uwazi Mizengwe, tukio hilo la aina yake, lilitokea mishale ya saa moja kasoro za jioni, Jumatano ya Aprili 22, 2015 kwenye eneo maarufu la Mwisho wa Lami zilipo ofisi za Chadema wakati Chenge na wafuasi wake wakirejea kutoka kwenye mkutano wa hadhara.
“Yaani ni Mungu tu, hivi sasa tungekuwa tunazungumza mengine kuhusu Mheshimiwa Chenge, wafuasi wa Chadema wangemuua,” alisema shuhuda wa tukio hilo aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini na kuongeza:
“Unajua siku hiyo kulikuwa na mikutano miwili ya hadhara, mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika eneo la Isanga na kuhutubiwa na Mheshimiwa Chenge na mwingine wa Chadema uliohutubiwa na John Mnyika na Heche.
“Mikutano yote iliisha salama na wafuasi wa Chadema wapatao 2,000, wakawasindikiza viongozi wao kwenda kwenye ofisi za Chadema zilizopo Mwisho wa Lami, kandokando ya Barabara ya Maswa- Lamadi,” alisema shuhuda huyo na kuendelea kuongeza kuwa walipofika kwenye ofisi hizo, waliendelea kuimba na kushangilia na kutawanyika mpaka barabarani.
“Ghafla msafara wa Chenge ukafika eneo hilo huku muziki ukisikika kwa sauti kubwa ndani ya gari moja, wafuasi wote wa Chadema wakiwa wameshika mawe wakauzingira na kuanza kuzomea. Mara Chenge na wafuasi wake wakateremka chini, hapo ndipo kiliponuka.
“Mtu mmoja aliwaamrisha wafuasi wa Chadema kuanza kuwapiga mawe watu wote, akiwemo Chenge, kukatokea bonge la mtiti, Chenge na wenzake wakawekwa ‘mtu kati’ na kutaka kushushiwa kichapo.
MILIO YA RISASI
“Ghafla ikasikika milio ya risasi tatu, watu wote wakatawanyika huku wengine wakikanyagana na kuwapa mwanya Chenge na wenzake kukimbilia kwenye magari yao na kutokomea kusikojulikana, yaani ilikuwa kama filamu ya mapigano vile, aisee,” alisema shuhuda huyo.
Baada ya kupata habari hizo, Uwazi Mizengwe liliwatafuta Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika na Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) John Heche kutaka kujua kilichotokea.
Kwa mujibu wa Mnyika, wao walikuwa kwenye ofisi za Chadema lakini ghafla walivamiwa na msafara wa Chenge ukiwa kwenye magari zaidi ya sita huku wakiwa wanapiga muziki kwa sauti kubwa na kuanza kufanya vurugu kabla ya mtu mmoja kwenye msafara huo kuchomoa bastola na kufyatua risasi.
“Ni kweli, ilikuwa ni baada ya mkutano mkubwa viongozi wa Chadema, walisindikizwa na wananchi mpaka kwenye ofisi zetu, Chenge na wenzake wakaamua kuja jirani na ofisi hizo na kufyatua risasi kuwatawanya wananchi,” alisema Mnyika na kumtaka mwandishi awasiliane na Heche ambaye ndiye aliyeenda kuandikisha maelezo kituo cha polisi.
Uwazi lilimtafuta Heche kwa njia ya simu na alipopatikana, alitoa maelezo ambayo hayatofautiani na Mnyika.
“Chenge na wafuasi wake walituvamia ofisini kwetu na kuanza kuleta fujo, ghafla tukashangaa wanatufyatulia risasi, ikabidi wafuasi wa chama chetu wakimbie kuokoa maisha yao,” alisema Heche na kuendelea kueleza kuwa baada ya tukio hilo, walikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Bariadi na kupewa RB yenye namba BAR/RB/1195/2015.
“Cha ajabu tulipofika kituoni, tulimkuta Chenge na wafuasi wake nao wamekuja kutoa taarifa,” alisema Heche.
CHENGE SIMU YAKE VP?
Uwazi Mizengwe halikuishia hapo, lilimtafuta Chenge ambaye muda wote simu yake haikuwa ikipatikana hewani. Likaamua kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, ACP Gemini Mushi ambaye alikiri kutokea kwa tukio hilo.
ASEMAVYO RPC
“Taarifa zilizopo ni kwamba Mheshimiwa Chenge na wenzake walikuwa wakitoka kwenye mkutano halali walioufanya eneo la Isanga, sasa wakati wanarudi wakapita kwenye ofisi za Chadema zilizopo Mwisho wa Lami ambapo wafuasi wa Chadema waliwavamia na kusababisha vurugu kubwa.
“Katika kujihami, mtu mmoja aliyekuwa kwenye msafara wa Chenge aitwaye Ahmed Ismail alifyatua risasi tatu hewani, ndipo wakapata upenyo wa kukimbia baada ya wafuasi wa Chadema kutawanyika.
“Mkanganyiko uliopo ni kwamba CCM wanasema Chadema ndiyo waliowavamia, Chadema nao wanasema CCM ndiyo waliowavamia, hivyo hali ni tete. Tunaendelea kulichunguza tukio hilo,” alisema Kamanda Gemini na kuongeza:
“Wanasiasa wajifunze kupambana kwa hoja wawapo kwenye majukwaa ya siasa lakini siyo kupigana kwa mawe au bastola.”
Kamanda huyo aliongeza kuwa baada ya kufanya uchunguzi, walibaini kwamba bastola iliyotumika, ilikuwa ikimilikiwa kihalali na Ahmed na kwamba hakukuwa na mtu yeyote aliyejeruhiwa.
Post a Comment