Loading...

WAANDISHI WA HABARI RUVUMA WAPIGWA MSASA JUU YA UZURI NA UBAYA WA UCHIMBAJI MADINI YA URANI

Asasi 3 zisizo za kiserikali leo zimetoa elimu kwa waandishi wa habari mkoani Ruvuma juu ya uelewa wa uchimbaji wa madini ya urani. Asasi hizo ni Caritas, MVIWATA Ruvuma na TMMTF.


Elimu iliyotolewa kwa waandishi hao wa habari ni kuimarisha elimu ya ushawishi kwa jamii katika faida na madhara ya madini ya urani, pia utafiti wa kisayansi ili kuainisha faida na madhara ya urani kwa binadamu na mazingira.


Katika semina hiyo uchimbaji wa madini umeonekana kuwa na madhara zaidi kuliko faidi kwa Watanzania. Habari zaidi itawajia muda mfupi.

Mr. Martine kutoka Ujerumani ni mmoja kati ya watoa mada



Mr. Martine na Mr. Mahundi wakujadiliana



Mr. Mahundi akitoa mada juu ya uandishi wa habari za kiuchunguzi



Ally Mzava kutoka CESOPE Dodoma akitoa mada juu ya uzoefu wa kuelimisha wananchi kuhusu athari za madini ya urani



Mr. Jeremia Araka mhadhiri wa chuo kikuu AJUCO akitoa mada juu ya misingi na maadili ya uandishi bora wa habari



Mr. Brito Mgaya akiwasilisha moja ya mada juu ya athari za madini ya urani



Mwandishi wa habari wa RFA Ngahyona Nkondora akiuliza swali kwa watoa mada


Joyce Kalinga mwakilishi wa TMMTF


Mwambije mwandishi wa habari wa ITV


Nathan Mtega - ITV


Gideon Mwakanosya - NIPASHE


Tamimu Gillo - Radio Jogoo Songea


Geofrey Nilai - Radio Maria



Waandishi wa Habari wakimfuatilia kwa makini mtoa mada


Mr. Yazidu Athuman mkazi wa Namtumbo jirani na mgodi wa urani akielezea kwa uchungu athari walizoanza kupata kabla uchimbaji haujaanza



Waalamu wa asasi zilizoandaa semina kwa waandishi wa habari wakifanya tathimini ya semina



Waandishi wa habari wakifanya tathimini ya semina

KIONGOZI WA WASABATO DUNIANI AJA TANZANIA


 
Kiongozi wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) duniani, Askofu Ted Wilson anatarajiwa kuwasili nchini leo kwa ziara ya kikanisa ya siku nne. 
Taarifa iliyotolewa na kanisa hilo, jijini Dar es Salaam, inaonesha kuwa kiongozi huyo anakuja nchini kushiriki Sherehe za Utume zilizoandaliwa na kanisa hilo na kujumuisha nchi zingine 11 za Afrika Mashariki na Kati.
Pamoja na kushiriki kwenye sherehe hizo, lakini kiongozi huyo atashiriki kwenye kuzindua miradi mbalimbali ya afya na elimu ya kanisa hilo nchini.
Sherehe hizo ambazo zinatarajiwa kuvuta zaidi ya watu 50,000 kutoka nchi hizo 11 na sehemu zingine duniani, zitakwenda sambamba na utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii, ikiwa ni pamoja kupima afya kwa magonjwa mbalimbali kama ya moyo, sukari, Ukimwi na magonjwa mengine.
Juzi Kiongozi wa Mawasiliano wa kanisa hilo katika ukanda wa Kati na Mashariki mwa Afrika, Mchungaji Steven Bina alisema mkutano huo wa siku nne, ambao unafanyika Uwanja wa Taifa ni wa aina yake na wa kwanza kufanyika nchini.
Katika mfululizo wa sherehe hizo, jana kulizinduliwa ujenzi wa Makao Makuu ya Jimbo la Kusini Mashariki mwa Tanzania (SEC), ambayo yatajengwa katika maeneo ya Kwembe, nje kidogo ya Dar es Salaam.
Shughuli zingine ambazo zilifanyika juzi ni uzinduzi wa kituo cha vitabu, ambacho kipo eneo la Ilala na kitatoa huduma kwa wakazi wa Dar es Salaam, ambao watahitaji vitabu mbalimbali vikiwemo vya afya na aina vya vyakula vinavyofaa kwa mwili wa binadamu. Kituo hicho kilizinduliwa na Mkurugenzi wa Idara ya Uchapishaji ya kanisa hilo duniani, Mchungaji Howard Faigao.
Miongoni mwa shughuli zingine ambazo zitafanywa na kanisa leo ni utoaji wa vitabu 1,000 na jozi 300 za viatu kwa ajili ya shule za msingi, na utoaji wa vifaa vya maabara kwa ajili ya shule za sekondari. Vitu hivyo vitatolewa kwa manispaa ya Ilala, ambayo ndio itakayovisambaza mahali ambako kuna mahitaji.
Mkutano huo unahusisha washiriki kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Eritrea, Somali, Ethiopia, Sudan Kusini na Djibout. Baadhi ya kwaya pia zitatoka nje ya Bara la Afrika.
Tamasha hilo kubwa la kitume, linatarajiwa kuhutubiwa kesho na Rais Jakaya Kikwete. Lakini pia kutakuwepo na viongozi wengine wapatao 400 wa kanisa hilo kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Sherehe hizo zenye kauli mbiu ya “Kusherehekea Mibaraka ya Mungu katika Utume”, zinafanywa na kanisa hilo ikiwa ni njia ya kujivunia mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika upelekaji wa injili na utoaji wa huduma za jamii.

AFISA ELIMU MBINGA AVULIWA MADARAKA


BARAZA la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma limemvua madaraka afisa elimu msingi wa wilaya hiyo Daniel Mkali baada ya kufanyiwa uchunguzi kwa muda kwa tuhuma mbalimbali zilizotajwa na baadhi ya madiwani pamoja na viongozi wa idara hiyo ya elimu msingi na kuelekea kutishia kuibuka kwa mgogoro wilayani humo.

Akitangaza uamuzi huo wa kumvua wadhifa huo pamoja na kumshusha cheo na kutakiwa kupangiwa shule ya kufundisha mwenyekiti wa halmashauri hiyo ya Mbinga Alanus Ngahi, mbele ya madiwani pamoja na watumishi wengine wa halmashauri hiyo amesema uamuzi huo umefikiwa na kamati ya maadili iliyokutana kujadili suala hilo la kinidhamu na kiutumishi na baraza hilo kuridhia hatua zichukuliwe dhidi ya afisa elimu huyo.

Akizitaja tuhuma nne zilizokuwa zikimkabili afisa elimu huyo, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Hussein Isa amesema ni pamoja na kusajili asasi isiyokuwa ya kiserikali iliyojulikana kwa jina la (UWEKAMBI) umoja wa waratibu elimu kata ya Mbinga na kuwaagiza walimu wakuu wa shule za msingi wilayani humo kuhamishia fedha zote za capitation na michango ya Umitashumta jumla ya shilingi milioni 232 ambapo katika fedha hizo shilingi milioni 60 ni michango ya Umitashumta, milioni 10 ni michango ya wazazi na shilingi milioni 61 ni fedha kwa ajili ya capitation na mitihani zilipelekwa kwenye akaunti yenye namba 61714000405 iliyopo katika benki ya NMB tawi la Mbinga.



Ameitaja tuhuma nyingine kuwa ni kughushi nyaraka kwa lengo la kutoa fedha kupitia ununuzi wa mafuta ya diesel lita 5500 na petrol lita 5500 na kuwaagiza walimu wakuu wachangie fedha za kupiga picha wanafunzi wa darasa la saba pamoja na fedha kwa ajili ya TSM 9 kwa maelekezo hayo ni kosa kwa sababu alikuwa akijua kuwa gharama za TSM 9 hugharamiwa na serikali kwa asilimia mia moja.

Amesema kati ya fedha hizo kiasi cha shilingi milioni 12.47 zilipelekwa kwenye akaunti hiyo ya UWEKAMBI na ameitaja tuhuma nyingine kuwa ni kumdanganya mwajiri kuwa hakujakusanywa fedha yoyote kutoka kwa wazazi na hakuna fedha ya capitation iliyopelekwa kwenye akaunti hiyo ya UWEKAMBI.

Aidha mkurugenzi mtendaji amesema baada ya maamuzi hayo yaliyotolewa na baraza la madiwani hatua nyingine zinazohusishwa na mamlaka nyingine zikiwemo za kinidhamu zitafuata ingawa kwa sasa anapaswa kuyatumikia maamuzi yaliyotolewa na baraza hilo la madiwani.

MBUNGE CCM AMVAA PINDA



Mbunge wa Bukoba Mjini kwa tiketi ya CCM, Khamis Kagasheki amemtuhumu Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwa ndiye aliyekuza mgogoro wa Bukoba uliosababisha madiwani wa halmashauri kushindwa kufanya vikao, akidai kuwa mtendaji huyo mkuu wa Serikali ameshindwa kuchukua hatua. Pinda hakuweza kupatikana, lakini msemaji wake alisema Waziri Mkuu ameshalishughulikia suala hilo kwa kiasi kikubwa.
Tuhuma hizo za Kagasheki ni za nadra kwa mbunge huyo wa chama hicho tawala kuelekeza kwa mtendaji mkuu wa Serikali na mmoja wa wajumbe wa vikao vya juu vya CCM.
Kagasheki, ambaye alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, alitoa tuhumu hizo wakati wa mahojiano maalumu na gazeti hili wiki iliyopita, akisisitiza kuwa ni makosa kuutazama mgogoro huo kuwa ni kati ya yake na meya na akataka ijulikane kuwa kinachoendelea Bukoba ni suala la wizi.
Mgogoro huo wa kisiasa, ambao umedumu kwa takriban miaka miwili na unaotishia kugawanyika kwa CCM, umekolezwa na kufunguliwa kwa kesi tatu ambazo zimezuia utekelezaji wa shughuli za maendeleo na umekuwa ukihusishwa na vita vya ubunge baina ya Kagasheki na Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kupata nafasi ya kuzungumzia suala hili. Hakuna unafiki hapa, hili nitalisimamia mahali popote na nitalisema mahali popote kuwa Pinda, ndiye tatizo katika mgogoro huu ulioinyima Bukoba maendeleo,” alisema Kagasheki.
“Lakini hiyo hainizuii kusema kuwa Tamisemi ndiyo tatizo, ingawa waziri wake ni Hawa Ghasia. Pinda ndiye msimamizi na bungeni alisema Amani siyo meya tena, lakini hakuna lililofanyika hadi leo na wananchi wanakosa maendeleo,” aliongeza akirejea kauli ya Pinda bungeni kuwa meya huyo alijiuzulu halafu siku chache baadaye Amani akaibuka na kukanusha habari za kuachia kiti cha umeya.
Alisema kuwa awali wakati mgogoro huo unafukuta, uongozi wa juu CCM uliagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG) kwenda Bukoba, naye akaenda kufanya utafiti, akamaliza na akatoa kila kitu.
Kagasheki alieleza: “ Nilikwenda katika kikao cha CCM, Pinda yupo ndani ya chama, kikaagiza madai hayo yafanyiwe kazi, lakini mpaka leo Takukuru hawajafanya chochote. Ndiyo maana nasema, Pinda akija kuomba kura (za urais) Bukoba, pale mjini, hali ni ngumu kwelikweli, atapata shida sana.
“Huu siyo mgogoro, ni wizi wa fedha na ripoti ya CAG ipo wazi lakini wahusika walio chini ya Waziri Mkuu hawataki kuifanyia kazi…Jambo hili lisipofanyiwa kazi, lazima itakuwa ajenda katika Uchaguzi Mkuu.”
Mbunge huyo wa Bukoba Mjini alisisitiza akisema: “Unajua kuna vitu vinaumiza, maana vile siyo vitu vyangu ni taarifa ya CAG na kwa kweli huyu CAG aliyeondoka ungekuwa unamuuliza ukweli, angekwambia amegundua mambo mengi ndani ya Serikali ambavyo hayafanyiwi kazi. Wizi usio na kifani, upotevu wa fedha na jambo zuri ni kuwa ile kazi aliyokuwa akafanya CAG ipo kikatiba.”
Alisema kuwa CCM ilitoa maelekezo na kupitia Serikali ikayapeleka Tamisemi, lakini hadi sasa hakuna pendekezo hata moja la CCM wala CAG lililofanyiwa kazi, lakini Waziri Mkuu yupo kimya.
“Tunapozungumzia Tamisemi, tunazungumzia Waziri Mkuu, bahati nzuri yeye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM. Uamuzi wa Kamati Kuu, Pinda hakufanya hata moja na hapo ndipo mgogoro ukapamba moto,” alidai.
MWANANCHI

AJALI MBAYA YATOKEA KIHESA IRINGA WATU WATATU WAFA NA KUWAKA MOTO





Ajali mbaya imetokea huu wa usiku Mjini Iringa eneo la kihesa Kilolo baada ya watu watatu waliokuwa kwenye bodaboda kugongana na lori aina ya fuso iliyokuwa inatoka mjini Iringa kuelekea Dodoma ktk barabara ya Iringa -Dodoma na wote watatu wamekufa eneo la tukio kwa kuwaka moto pamoja na piki piki yao picha hazifai.
cdt: mzee wa matukio

Haya Ndio Maisha aliyopitia Mh January Makamba Toka Anazaliwa Mpaka Hapo Alipofikia!





Nilizaliwa tarehe 28 Januari 1974 mjini Singida, kwa Bi. Josephine Joseph na Bwana Yusuf Makamba. Mwaka 1978, nilipelekwa kuishi kijijini kwa bibi mzaa mama Kyaka, Kagera wakati mama ameenda kuendelea na masomo ya uuguzi. Kijijini kwetu ilikuwa umbali mfupi kutoka Mutukula, mpakani mwa Tanzania na Uganda. Idi Amini alipovamia Tanzania mwaka huo, kitongoji chetu kinachoitwa Kituntu, sio Kituntu ya Karagwe unayoijua wewe Padre, karibu na Kyaka nacho kilipigwa mabomu. Mimi na bibi yangu tulikimbia makazi yetu na kuhamia kwenye kambi ya wakimbizi eneo linaloitwa Mwisa. Baba yangu wakati huo alikuwa mstari wa mbele kwenye vita dhidi ya Idi Amin. Tulikaa kambini kwa muda baadaye tukafanyiwa utaratibu wa kuondoka kwenda Biharamulo na mama akaja kutuchukua. Sina kumbukumbu kubwa sana ya kipindi hiki kwa kuwa nilikuwa bado mdogo ila nakumbuka mvua nyingi, milio ya ndege na mabomu.

Nimesoma shule nne za msingi katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu kutokana na wazazi kuhamishwa mara kwa mara katika utumishi wa umma. Lakini pia kuanzia darasa la tatu hadi la tano nilirudishwa tena kijijini, Kituntu Kyaka, kukaa na bibi. Maisha ya kijijini siwezi kuyasahau. Enzi hizo, miaka ya mwanzoni mwa 1980, maisha ya kijijini yalikuwa magumu sana, bidhaa muhimu kama sukari, sabuni, dawa za mswaki, chumvi, na nyinginezo, zilikuwa adimu. Kutoka kitongojini Kituntu hadi shuleni ilikuwa mwendo mrefu na baada ya shule nilikuwa na kazi ya kwenda kuchunga mbuzi wa bibi, na baada ya kuchunga mbuzi kila jioni saa moja ilikuwa ni kazi ya kuchota maji mtoni, na baada ya hapo ilikuwa ni kumsaidia bibi kuuza pombe ya lubisi usiku na Jumamosi ilikuwa ni kwenda shamba kupalilia migomba na mikahawa. Maisha yale yalinifundisha mambo mengi. Baada ya miaka mitatu, nilirudi kukaa na wazazi na kumalizia darasa la saba Shule ya Msingi Masiwani, Tanga Mjini.

Nilianza Sekondari katika shule ya Sekondari Handeni, Tanga. Nakumbuka wakati naanza pale shule ile ilikuwa bado inajengwa, sisi tulikuwa Form 1 wa pili na ilikuwa haina tofauti kabisa na shule ambazo sasa zinaitwa shule za Kata. Kwa kuwa hii ilikuwa shule ya kutwa, mzazi wangu alipohamishwa kikazi kutoka Handeni, nikahamia Shule ya Sekondari Galanos Tanga, ambayo ilikuwa shule ya Serikali ya boarding.

Nilikuwa mwanafunzi mzuri pale Galanos, na, nikiwa kidato cha tatu, nikachaguliwa kuwa Makamu wa Kiranja Mkuu. Nilikuwa nafanya vizuri darasani, nikachagua mchepuo wa sayansi nikiwa na combination ya Chemistry (Kemia), Biology (Baiolojia) na Agriculture (Kilimo) (CBA). Nilipata daraja la kwanza kwenye mtihani wa kanda wa mock wa kidato cha nne, nikiwa na uhakika wa kuendelea na A-Level katika Shule ya Sekondari Kibaha, shule pekee iliyokuwa inafundisha mchepuo wa CBA hapa nchini. Hata hivyo, nilifanyiwa hujuma kubwa kutokana na siasa zinazomhusu Mzee wangu na kufutiwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne.

Sikufa moyo, nilirudia mtihani kama mtahiniwa binafsi na kufaulu na kuweza kusoma A-Level katika Shule ya Sekondari Forest Hill Morogoro na nikapata Daraja la Pili kwenye mtihani wa Kidato cha Sita. Kabla ya kwenda Chuo Kikuu, niliamua kwenda kufanya kazi kwenye makambi ya wakimbizi kutoka Burundi yaliyokuwa wilaya ya Kasulu, Mkoani Kigoma. Niliipenda sana kazi ile ya kuhudumia wakimbizi na kuifanya kwa bidii kubwa. Nilipewa madaraka zaidi hadi kufikia nafasi ya Meneja wa Kambi Msaidizi wa Kambi ya Mtabila 2 iliyokuwa na wakimbizi zaidi la laki moja. Nilibahatika kuwa na wajibu na dhamana kubwa ya kuongoza kambi kubwa na wafanyakazi wengi nikiwa na umri mdogo tu wa miaka 21. Nilikuwa na wafanyakazi wengi, tena wengine watu wazima, waliokuwa wanaripoti kwangu. Nilikuwa na wajibu wa kuhakikisha kwamba wakimbizi laki moja wanapata viwanja vya kuishi, wanapata vifaa muhimu kama mahema, na wanapata chakula. Kazi ile ilibadilisha kabisa mtazamo wangu juu ya maisha. Baada ya kushuhudia adha wanayopata wanadamu wenzetu kutokana na vita hadi kukimbia makazi yao na nchi yao na kuja kukaa maporini kwenye nchi yetu, na baada ya kutafakari kuhusu udhalilishwaji na mateso yanayotokana na ukimbizi, niliamua kuachana na azma ya kusoma sayansi na uchumi na nikaamua kwamba maisha yangu nitayatoa katika kuchukua masomo kuhusu amani, na namna ya kutafuta amani ili nitoe mchango kwenye kuepusha vita na kupatikana kwa amani duniani. Hivyo, nilianza kutafuta vyuo duniani vinavyofundisha masuala ya amani. Nilipata chuo kimoja cha Wakatoliki Marekani, kinachoitwa St. John University. Lakini kilikuwa Chuo aghali kidogo, kwa hiyo nikaanza kusoma masomo ya awali kwenye Chuo kingine kidogo katika jiji la Boston kinachoitwa Quincy College na baadae nikajiunga na St. John University na kupata shahada ya kwanza ya sayansi ya masomo ya amani (Bachelor of Science in Peace Studies). Gharama za masomo zilikuwa kubwa na nilihangaika kufanya kazi mbalimbali, ikiwemo kazi za ulinzi na kuhudumia watu wenye magonjwa ya akili ili kulipia ada ya shule.

Baada ya kumaliza shahada ya kwanza, nilishinda tuzo ya kujiunga na taasisi ya Rais Mstaafu wa Marekani, Jimmy Carter, inayoitwa Carter Presidential Center iliyopo Atlanta hukohuko Marekani. Ilikuwa changamoto kubwa na fursa nzuri kwa sababu vijana wote waliojiunga pale walikuwa ni vijana mahiri sana na wenye uwezo mkubwa. Taasisi ile ilinipeleka nchini Sierra Leone kusimamia uchaguzi mkuu na kutekeleza mradi wa kufufua taasisi za haki zilizoporomoka baada ya vita. Nako pia nilijifunza mengi kuhusu ujenzi wa taifa.

Baada ya hapo nikaamua kuchukua shahada ya pili (Masters degree) kwenye Chuo Kikuu cha George Mason kilichoko Jimbo la Virginia, Marekani. Nilipata wakati mgumu kulipa ada, kiasi cha kukaribia kufukuzwa shule. Niliomba msaada kwa watu mbalimbali akiwemo Rais wa wakati ule Mhe. Benjamin William Mkapa. Bahati nzuri, alikubali kusaidia kwa sharti kwamba nije kutumia utaalamu wangu Serikalini nitakapomaliza masomo. Na ndivyo nilivyofanya. Baada ya masomo hayo, nikajiunga na Wizara ya Mambo ya Nje.

Mwaka 2005 nilifunga ndoa na mchumba wangu wa miaka minne, Ramona Urasa, na nimekuwa na familia yenye furaha sasa mwaka wa kumi. Pale Wizarani, nilipata fursa ya kufanya kazi na Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete. Nahisi alipenda kazi zangu na mara alipoamua kuwania nafasi ya Urais akanitaka nichukue likizo isiyo na malipo Serikalini ili niwe msaidizi wake kwenye kampeni zile. Siwezi kusahau maishani mwangu ile fursa kubwa kwani niliweza kuijua kwa kina nchi yangu na watu wake. Na kwa kuwa kampeni zinahusu ahadi za utatuzi wa kero za watu, nilipata fursa ya kujua kero za Watanzania kwenye kila wilaya ya nchi yetu.

Baada ya Rais Kikwete kushinda aliniteua kuwa Msaidizi wake Ikulu, nikiwa na jukumu la kumsaidia kuandika hotuba zake, pamoja na mambo mengine mengi ya uendeshaji wa shughuli zake za kila siku. Kazi ile ilikuwa ngumu kwa sababu inakulazimisha kujifunza na kujua karibu kila kitu ndani ya Serikali na duniani kwa ujumla, na kufanya utafiti karibu kila siku kwa sababu Rais anazungumza kila siku kuhusu mambo mbalimbali na kwa makundi mbalimbali. Pia kazi ile inakupa fursa ya kuhudhuria vikao vya Baraza la Mawaziri kama msikilizaji ambapo pia unajifunza mambo mengi ya uendeshaji wa Serikali, ikiwemo maamuzi muhimu ya kisera na kiutendaji yanavyofanywa. Ni nafasi ya heshima sana na sitamsahau Rais Kikwete kwa kunipa fursa ile.

Baba yangu alikuwa mwanasiasa karibu maisha yake yote lakini sikupata kuwaza kuingia kwenye siasa katika maisha yangu hadi nilipofanya kazi na Rais Kikwete. Baada ya kufanya kazi ile Ikulu kwa miaka mitano, nami nikahamasika na kuamua kushiriki katika uongozi wa umma. Niliamua kwenda kwetu Bumbuli kugombea nafasi ya Ubunge mwaka 2010, nikafanikiwa. Baada ya kuingia Bungeni nikapata nafasi ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini. Kazi ile tuliifanya vizuri sana na wenzangu kwenye Kamati hasa katika kipindi kile kigumu cha mgao wa umeme na matatizo ya mafuta nchini.

Baada ya kitambo kidogo, nikateuliwa kwenye Sekretarieti ya Chama nikiwa kama Katibu wa NEC wa Siasa na Mambo ya Nje, na nikawa Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM. Nilishika nafasi hizi katika kipindi kigumu sana kisiasa kwa Chama chetu na nilijifunza mambo mengi na kutoa mchango wangu kwenye kukijenga na kukiimarisha. Baada ya kitambo kingine, nikateuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.

Kuhusu kubebwa na jina la mzazi, kama nilivyosema hapo awali, pamoja na kwamba mzazi wangu alikuwa kwenye siasa kwa muda mrefu, binafsi, ingawa nilipenda na nilishiriki kuwa kiongozi tangu shuleni, sikuwa na mawazo ya kuingia katika siasa. Nilipokuwa Sekondari nilipenda kuwa mwanasayansi wa kilimo.

Baada ya kuzunguka nchi nzima kwenye kampeni ya 2005 na baada ya kufanya kazi ya kumsaidia Rais Ikulu ndipo nilipobaini kwamba siasa, ukiiendesha vizuri na kwa manufaa ya watu, inayo nafasi ya kubadilisha maisha ya watu. Nilipofanya uamuzi wa kugombea Ubunge, sikutaka ushauri wa baba yangu kwa sababu nilikuwa na uhakika kwamba angenikatalia. Niliamua mwenyewe na nikaanza harakati na ndipo nikamwambia. Kwa hiyo, unaweza kuwa na mzazi mwanasiasa na bado ukaweza kuwa na uhuru wa kujiamulia mwenyewe unataka kufanya nini.

Ni kweli kwamba jina maarufu la mzazi aliye kwenye siasa linasaidia kwa maana tayari kuna watu ambao wanamheshimu na ambao wapo tayari kukusaidia. Lakini pia jina hilohilo linaweza kukuharibia kwa sababu pia unaweza kurithi maadui zake, ambao wanakuona wewe ni sehemu ya yeye hata kama una mawazo na mtizamo huru. Kwa hiyo, siasa yangu nimejitahidi kuifanya kama mimi binafsi. Mimi na baba yangu tuna staili tofauti za siasa na mimi nina namna yangu ya kufanya mambo ambayo inatofautiana na yake. Lakini pia kuna mambo mengi mazuri ambayo nimejifunza kutoka kwake ikiwemo haja ya kuwa na msimamo usioyumba katika unayoyaamini na haja ya kutokumuogopa mtu yoyote.
Newer Posts Older Posts
© Copyright Bongo Mirror | Designed By BONGOJAMII.COM
Back To Top